Mafunzo hayo yametolewa kwa madereva hao ambao wengi wao hawakuwa na mafunzo ya udereva ikiwa ni mkakati wa serikali kupunguza ajali zinazotokana na uendeshaji wa vyombo vya moto bila kuwa na mafunzo.
Wahitimu wa mafunzo hayo walitunukiwa vyeti pamoja na kupewa leseni za udereva katika hafla iliyofanyika mkoani Kilimanjaro na kuhudhuliwa na mkurugenzi Mkuu wa LATRA ,CPA Habib Suluo sanjari na Naibu kamishina wa jeshi la polisi(DCP)Johanes Kahatano ambaye ni mkurugenzi wa Idara ya Barabara kutoka LATRA.
Madereva hawa wa bodaboda na Bajaji ni wanachama wa Chama Cha Akiba na mikopo(KIBABOT)ambao wamepata mafunzo ya namna ya kuendesha ushirika kutoka Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2022 hadi 2024 jumla ya wananchi 1,113 wamepoteza maisha kutokana na ajali za boda boda hii ni kwa mujibu wa Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Daniel Sillo.
Kwa mujibu wa takwimu hizo,jumla ya madereva wa boda boda 759 walipoteza maisha huku abiria wao 283 nao wakipoteza maisha huku wavuka barabara ama watembeaji wa pembezoni mwa barabara 71 nao wakipoteza maisha.
Akizungumza katika hafla hiyo,mkuu wa wilaya ya Moshi,Godfrey Mnzava kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Nurdin Babu amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kila mtumiaji wa chombo cha moto wanazingatia sheria,kanuni na taratibu za usalama barabarani.
Amesema uzingatiaji huo wa sheria,kanuni za usalama barabarani utaongeza nidhamu barabarani na kupunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la ajali za barabarani zinazopoteza nguvu kazi za vijana lakini pia kuongeza mzigo wa familia na serikali katika kuwahudumia majeruhi wa ajali hizo.

0 Comments