Makala haya yameandaliwa na Bahati Nyakiraria na Charles Ndagulla
Mkurugenzi wa Kampuni ya African Scenic,Elisimbo Natal(kushoto)akiwa kwenye picha ya pamoja na mmoja wa wapanda mlima kwenye kampeni ya Twenzetu Kileleni msimu wa 2024 Bahati Nyakiraria muda mfupi baada ya kuhitimisha safari ya siku nane ya kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
KILIMANJARO
SAA nane na nusu ya mchana ya Jumanne ya
Desemba 3 mwaka jana tulianza safari ya siku nane kuupanda mlima Kilimanjaro
kupitia lango la Lemosho lililopo magharibi mwa mkoa wa Kilimanjaro eneo la
West Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa
Tanganyika.
Hii ni baada ya kukamilika kwa zoezi la kuagwa
kwetu lililofanywa na Mkuu wa wilaya ya Siha,Christopher Timbuka na maofisa wa
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(Tanapa).
Safari hii ya kuuupanda mlima Kilimanjaro
ilikuwa chini ya uratibu wa kampuni ya wakala wa Utalii ya African Scenic moja
ya kampuni za uwakala wa utalii zenye uratibu mzuri kwenye sekta ya utalii.
Kundi letu la watu zaidi ya 30 lilikuwa na mchanganyiko
wa wapanda mlima wakiwamo waandishi wa habari,askari kutoka hifadhi mbalimbali za
taifa na kutoka Taasisi mbali mbali wakiwamo maofisa kutoka wakala wa Umeme
vijijini(REA)
Safari yetu ilikolezwa na nyimbo za hamasa
kutoka kwa vijana wa Tanapa wakiongozwa na Chacha na ilituchukua muda mfupi kukifikia
kituo cha kwanza cha Mti mkubwa kilichopo umbali wa mita 2,650 kutoka usawa wa
bahari,kituo hicho kipo ukanda wa msitu mnene wenye hewa ya kuvutia.
Hali ya hewa ilikuwa ya kuvuti ikichagizwa na mvua ya wastani na hapa wapishi walikuwa tayari wametuandalia chai ili kuondoa kiubaridi kabla ya kupata chakula cha jioni.
Siku ya pili Desemba 4 saa moja na nusu
asubuhi tukiwa na afya njema kabisa timu nzima tukiongozwa na waongozaji wageni
nguli kutoka African Scenic ,Joel Siao ,Alfred Kibiriti,Said Konde a.k.a Sinde
konde ,na mwanamama shupavu kabisa Mary Shayo tulianza safari yetu kuelekea
kituo cha pili cha Shira one Camp ummali wa Kilometa saba kutoka mti Mkubwa
ikituchukua mwendo wa saa nne kukifikia kituo hicho.
Ilikuwa safari ya damu na jasho kukifikia
kituo hicho,kuna wakati ukimya unatawala zile nyimbo za hamasa zinakata kwa
muda hasa eneo la mgongo wa tembo,hapa unahitaji utimamu wa mwili kukimaliza
kigongo hicho.
“Anayesema njia ya Marangu ni ngumu
mwakani aje apande huku aone hii safari ilivyo ya moto,ukitoboa hapa
unakutana na kigongo kingine kutoka Baranco kwenda Karanga,acha kabisa”,anasikika
akisema mmoja wetu.
Hapa Shira one Camp ni sehemu inayokupa uwanda
mzuri wa kufurahia mandhali ya mlima Kilimanjaro kutokana na kuwa na hewa nzuri
inayovutia.
Suala la afya ni moja ya vipaumbele vya kampuni hii ya African Scenic kwani kila baada ya chakula cha jioni kuna dodoso la kitabibu analojaziwa mgeni baada ya kufanyiwa mahojiano na kufanyiwa vipimo kwa wale wanaojisikia vibaya lengo ni kuhakikisha kila mgeni yupo vizuri kiafya na yupo tayari kwa zoezi la kuendelea na safari kwa siku inayofuata.
Magwiji hawa wa kupandisha wageni mlimani kutoka kampuni hii wanayo mafunzo ya awali kwa ajili ya utoaji wa huduma ya kwanza mafunzo ambayo wamekuwa wakipatiwa mara kwa mara na kampuni lengo ni kuwawezesha kuwahudumia wageni wao ipasavyo.
Kutoka Shira one Camp unaianza safari ya kukitafuta kituo cha tatu cha Shira II safari inayokuchukua muda wa saa nane na usheee kukifikia kituo hicho ukipanda na kushuka kwenye vilima tofauti huku ukikitazama kilele cha mlima Kilimanjro kwa ukaribu kabisa.
Ni safari inayokupa uhuru mpana wa kufurahia uumbaji wa mungu na Baraka za kuwa na vivutio vizuri kama mlima Kilimanjaro moja ya kivutio kikubwa cha utalii kinachovutia maelfu ya watalii kutoka kila kona ya dunia.
Kutoka Shira II Camp kuelekea Barango Camp ni safari inayohitaji uwe na utimamu wa mwili kweli kweli,ni safari inayokuwezesha kuona maeneo mengi mazuri na ya kuvutia ikikushusha chini kabisa mithiri ya kushuka bondeni huku kwa pembeni ikishuhudiwa maporomoko ya maji yanayotirirsha maji msimu mzima.
Kukifikia kituo hiki
unapitia makutano ya waliopanda mlima kupitia lango la Machame na Lemosho
kuelekea eneo la Lava Tower,hapa ni sehemu makundi yote yanapata chakula cha
mchana kabla ya kuelekea Baranco Camp.
Saa 12 tunafika kituo cha Baranco,kama kawaida tunapa chai ya jioni ya kupasha mwili japo tunachapwa na mvua ya kutosha kabla ya chakula cha jioni,zoezi la vipimo vya afya linaendelea kwa kila mpanda mlima lengo ni moja tu kila mmoja anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuendelea na safari siku inayofuata.
Desemba sita tunaanza safari yetu kutoka Baranco kuelekea Karanga Camp,hapa ndipo kila mtu anajua kumbe ndiyo kwanza naanza kupanda mlima Kilimanjaro,hapa unapita kwenye jiwe la ‘kubusu’vijana wa mjini wanasema weka mbali na watoto.
Kutoka Baranco kwenda kituo cha mwisho kabla ya kukwea Kileleni cha Barafu ni safari inayokupa mwanga mzuri wa kujua unakwenda Kileleni au unabaki Camp?,kila mmoja anashauku ya kufika Barafu Camp.
Kwa pamoja tunafika Barafu na kupata mapunziko kama kawaida kabla ya kuianza kuianza safari kuelekea kituo cha Kosovo lengo letu ni kupunguza umbali wa safari kuelekea Kileleni usiku wa deemba nane.
Hakika ni safari inayovutia kwa kila anayepata bahati ya kuupanda mlima Kilimanjaro na safari yetu hii ilikuwa ya mafanikio makubwa saana kwani idadi kubwa tuliweza kukifikia kilele hicho pendwa alifajiri ya deemba 9 .
Kila aliyebahatika
kukifikia kilele hiki alikuwa mwenye furaha isiyo kifani,kila mtu alikuwa
napiga picha ya ukumbusho kwenye kibao kabla ya kuanza safari ya kushuka chini
kupitia Millenium hadi Mweka Camp na siku ya desemba kumi tukafanikiwa kushuka
Mweka Gate na kuungana na wenzetu waliokuwa nji ya Marangu kwenye ofisi kuu ya
Kinapa.
Hakika Twenzetu Kileleni ni zaidi ya kupanda mlima Kilimanjaro
.jpg)











0 Comments