POLISI MBEYA WAMTIA MBARONI MTANZANIA AKISAFRISHA WAHAMIAJI HARAMU 38

 

JESHI la polisi mkoa wa Mbeya linamshikilia mtanzania mmoja Stanslaus Mazengo(51)mkazi wa Isitu mkoani humo akituhumiwa kusafrisha wahamiaji haramu 38 raia wa Ethiopia kwa kutumia gari lake dogo aina ya Toyota Noah lenye namba sa usajili T953DJF.

kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi mkoani Mbeya,wahamiaji hao haramu walikamatwa Novemba 11 mwaka huu katika pori la Lanchi ya Matebele lililopo katika kijiji cha Igumbilo mkoani Mbeya.

Kulingana na taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi mwandamizi wa polisi(SACP),Benjamin Kuzaga ,baada ya mahojiano dereva huyo alidai kuwa alikuwa akiwapeleka watuhumiwa hao kwenda kuwahifadhi kwenye nyumba ya Mwanamke mmoja(jina tunalihifadhi)katika eneo la Chimala.

Kulingana na taarifa ya jeshi la polisi,wahamiaji hao haramu walikuwa wasafrishwe kwa njia za panya na kuvuka mpaka wa Tanzania kwenda nchini Afrika kusini.

Mtandao wa kusafrisha wahamiaji haramu umekuwa ukihusisha watanzania wakishirikiana na raia wa nchi jirani ambako inadaiwa wamekuwa wakijiingizia fedha nyingi kupitia biashara hiyo haramu,

Hata hivyo,jeshi la polisi mkoani Mbeya limetoa rai kwa  wananchi wenye tamaa ya kujipatia fedha kuacha tabia ya kuwawezesha raia wa kigeni kuingia ama kupita nchini bila kufuata taratibu za kisheria na badala yake wawaelekeze kufuata taratibu kupitia mamlaka husika ili kuepuka usumbufu ikiwamo kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria .

 





Gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T953DJF linalodaiwa kutumika kusafrisha wahamiaji haramu 38 raia wa Ethiopia,gari hilo lilikamatwa na maofisa wa jeshi la polisi mkoani Mbeya 

Post a Comment

0 Comments