Makala
hii imeandaliwa na Bahati Nyakiraria na Charles Ndagulla 
Desemba 3 mwaka jana kundi la wapanda mlima 30 likijumuisha waandishi wa habari,lilianza safari ya siku nane kupanda mlima Kilimanjaro kupitia lango la Lemosho kwa usaidizi wa kampuni ya wakala wa Utalii ya African Scenic ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika .
Kundi la pili lilianza safari yake Desemba 4 kupitia lango la Machame kwa usaidizi ya kampuni ya wakala wau talii ya African Zoom na kundi la tatu na la mwisho lilianza safari yake Desemba 5 kupitia lango la Marangu kwa usaidizi wa kampuni ya wakala wa utalii ya Zara Tours.
Kundi hili la tatu lilihusisha askari wa jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ)maofisa wa vyeo vya juu wa JWTZ,Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi mbali mbali pamoja na maofisa kutoka Taasisi mbalimbali.
Askari hawa wa JWTZ walikuwa mahususi kwa ajili ya kuipeleka Bendera ya Taifa kwenye kilele cha uhuru ambacho kipo mita 5,895 kutoka usawa wa bahari kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika.
Hili ni tukio ambalo limekuwa likikua kila kukicha kutokana na kuwepo na mwitikio mkubwa wa watu ambao wamekuwa wakijitokeza kupanda mlima huo ambao ni wa kwanza kwa urefu afrika na ni mlima mrefu duniani uliosimama pekee.
Tukio
hili hubebwa na kampeni ya “TWENZETU KILELENI” na mwaka jana ulikuwa ni
msimu wake wa nne mfululizo tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2021 licha ya kwamba
ni tukio ambalo limekuwa likifanyika mara kwa mara tangu maadhimisho ya miaka
50 ya uhuru ambako kundi kubwa la watu zaidi ya 200 walipanda mlima huo.
Mrisho Salakikya mstaafu wa jeshi la wananchi Tanzania(JWTZ)ndiye chachu ya zoezi hili la kupanda mlima kilimanjaro akiongoza maofisa wa vyeo mbali mbali wa JWTZ kupanda mlima huo.
Baadae alikabidhi kijiti hicho kwa mkuu wa zamani wa JWTZ.George Waitara ambaye aliendeleza kampeni hiyo kabla ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa).
Katika miaka ya hivi karibuni,kampeni hii imeendelezwa na Tanapa kupitia kampeni hii ya "Twenzetu Kileleni"inayolenga kuhamasisha watanzania kupanda mlima kilimanjaro kama ishara ya uzalendo na kukuza utalii.
Mwaka jana kampeni ya “Twenzetu Kileleni”ilibeba ujumbe mzito wa kutunza mazingira ya mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuokoa barafu ya mlima huo ambayo ipo kwenye tishio la kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu.
Uharibifu wa mazingira unaoendelea kwa kasi, unahitaji umakini wa haraka, hasa katika maeneo yenye mazingira tete kama Mlima Kilimanjaro.
Barafu
ya mlima Kilimanjaro ni moja ya alama za kipekee za mazingira na mabadiliko ya
hali ya hewa duniani,kutoweka kwa barafu hii kunahusiana na mabadiliko ya hali
ya hewa, ambapo ongezeko la joto duniani linaathiri maeneo ya milimani kama
Kilimanjaro.
Mabadiliko
haya yanaathiri kwa namna moja au nyingine kwa sababu:
Ongezeko la joto:
Joto la dunia linapoongezeka, barafu na theluji za milimani zinayeyuka kwa haraka kwenye mlima Kilimanjaro, kutokana na joto la ulimwengu, limekuwa ni eneo ambalo barafu zake zinapotea kwa kasi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1912 na sasa,
Kilimanjaro imepoteza karibu 80% ya barafu yake hatua ambayo inahitaji msukumo
mkubwa kutoka kwa jamii ya watanzania na Taasisi za uhifadhi wa mazingira
katika kuokoa thuluji isitoweke.
Mabadiliko ya mvua:
Mabadiliko ya mifumo ya mvua pia yanachangia hali ya mvua inaweza kuwa isiyotabirika au kutosha, ambayo inaathiri kiwango cha theluji inayoongezeka au kutunzwa juu ya mlima.
Uharibifu wa mazingira:
Uharibifu wa misitu na shughuli za kibinadamu, kama ukataji
miti, uchimbaji madini na kilimo cha kukata, pia unasababisha kupungua kwa
unyevu wa hewa, hali inayochangia kuyeyuka kwa barafu.
Utalii
na shughuli za kibinadamu:
Utalii katika Mlima Kilimanjaro, kama vile kupanda mlima ni moja ya shughuli kubwa zinazofanyika kutokana na mlima huo kuwa sehemu kubwa inayoliingizia taifa fedha za kigeni lakini wataalamu wa mazingira wanasema shughuli hizo zinachangia uchafuzi wa mazingira na kuingiza kemikali zinazoweza kuharibu hali ya hewa na mazingira ya mlima.
Hili ni tishio kubwa kwa ikolojia ya mlima Kilimanjaro na pia kwa jamii zinazotegemea maji kutoka kwenye vyanzo vya barafu za mlima.
Pamoja na hayo, kupotea kwa barafu kunapunguza uwezo wa Mlima Kilimanjaro kutoa maji kwa mito inayopita chini ya mlima, ambayo ni muhimu kwa kilimo na maisha ya watu wanaoishi maeneo ya chini.
Hali
hii inahitaji hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa,
ulinzi wa mazingira, na usimamizi bora wa rasilimali za asili ili kuhakikisha
kwamba tunahifadhi barafu ya Mlima Kilimanjaro kwa vizazi vijavyo.
Ni hatua zipi zinahitajika kuhakikisha theluji ya mlima kilimanjaro haitoweki kutokana na tishio la kutoweka kwake kunakosababishwa na uharibifu wa mazingira unatokana na shughuli za kibinidamu?
endelea kufuatilia makala zetu kupitia ukurasa huu







0 Comments