Nehemiah Mchechu,Msajili wa Hazina
KILIMANJARO
SERIKALI imekiri kuridhishwa na uwekezaji mzuri uliofanywa na wawekezaji kwenye kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo mkoani Kilimanjaro huku ikijivunia gawio kubwa linalotolewa na kiwanda hicho kwa serikali kila mwaka.
Pongezi hizo zimetolewa na msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu muda mfupi baada ya uzinduzi wa ujenzi wa kongani ya viwanda unaofanywa na mwekezaji huyo uliofanyika kwenye kiwanda hicho.
Alisema TPC ni moja ya wawekezaji wanaofanya vizuri kwenye sekta ya viwanda na kwamba uwekezaji huo mzuri umefanya serikali kupata gawio kubwa mwaka jana la shilingi Bilioni 16.5 huku mwekezaji huyo akichangia zaidi ya shilingi Bilioni 75 mapato yote.
Kuhusu kongani hiyo ya viwanda,Mchechu alisema kiwanda kitakachojengwa kitazalisha Lita Milioni 16.3 za spirit kwa mwaka sawa na lita 65.000 kwa siku pamoja na uzalishaji wa Megawati 6 za umeme na mbolea inayotokana na mabaki ya miwa .
“Katika uzalishaji wa miwa huwa kuna mabaki sasa hayo mabaki na uchafu wote ndiyo tunakwenda kutengeza kiwanda ili kitengeneze spirit,tutakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 16.3 kwa mwaka sawa na lita 65,000 kwa siku lakini upanuzi huu wa kiwanda tunakwenda kuzalisha umeme kama megawati 6 lakini pamoja na hiyo katika uzalishaji wa kiwanda hiki uchafu wote na mabaki yote tunakusanya na kwenda kutengeneza mbolea”.
“Kwa hiyo unakuta kwamba katika uwekezaji wa kiwanda hiki siyo tu tutapata spirit lakini pili mpaka mbolea na umeme maana yake uchafu wote unarudi na kuwa na manufaa zaidi, hawa ni wawekezaji ambao tunafuraha kuwa nao “
Amesema uwekezaji huo
una manufaa makubwa kwa serikali kwani shamba hilo lilikuwa linakwenda kufa
lakini kwa sasa kupitia mwekezaji huyo kuna wafanyakazi zaidi ya elfu nne
wameajiliwa na kusisitiza serikali inahitaji wawekezaji wa aina hiyo.
Kwa ujumla ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji katika kiwanda cha hicho cha sukari cha TPC umepelekea mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, na kuifanya kampuni hiyo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu katika sekta ya viwanda.
TPC iliandaa chakula cha jioni ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 ya mafanikio na ushirikiano muda mfupi baada ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo mkubwa kiwanda kipya cha kuchakata molases ‘TPC Distillery’ wenye lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kupanua wigo wa viwanda.
Kuzinduliwa kwa ujenzi wa mradi huo ni hatua muhimu katika upanuzi wa TPC, ambapo unatoa fursa ya upanuzi wa shughuli za kampuni katika utengenezaji wa Extra Neutral Alcohol (Ethanol), mbolea ya potasiumu, na nishati mbadala, huku ukichangia zaidi ya megawati sita (6 MW) kwenye gridi ya taifa.
Ushirikiano kati ya serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), na TPC ulianza wakati serikali ilipobinafsisha TPC Limited kwa kuuza asilimia 75 ya hisa zake na kubakisha asilimia 25, jambo lililoacha mlango wazi, kwa uwekezaji mpya, utawala wa kisasa na ukuaji wa muda mrefu.





0 Comments