MLIMA KILIMANJARO KAMA UNAVYOONEKANA
SAFARI ya kuupanda mlima Kilimanjaro ambao ndiyo mlima mrefu kuliko yote barani afrika,haihitaji mbwembwe bali ni utimamu wa mwili,afya njema na kufuata maelekezo ya waogazaji wageni.
Hiyo ndiyo siri ya mafanikio kwa wale
wanaofanikiwa kukifikia kilele cha Uhuru kilichopo mita 5,895 kutoka usawa wa
bahari licha ya changamoto za hapa na pale yakiwamo mabadiliko ya hali ya hewa.
Ili upande mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele cha uhuru,unahitaji ushirikiano wa watu watatu ambao ni waongozaji wageni(guide), wapishi na wabeba mizigo ya wageni ambao wanajulikana kwa jina la wapagazi ama kwa jina maarufu wagumu.
Ni ukweli usiopingika kwamba watu hawa watatu ndiyo tumaini kubwa la mgeni yoyote anayepanda mlima huo kwani kila mmoja wao ana umhimu mkubwa kulingana na eneo lake la kazi.
Mwongozaji wageni
Mwongozaji wageni(guide) na msaidizi wake
hawa ndiyo wanaoweza kumfikisha mgeni katika kilele cha
uhuru kutokana na maelekezo wanayoyatoa kwa
wageni kuanzia mwanzo wa safari hadi mwisho wa safari.
Ni watu ambao wanamwelekeza mgeni afanye nini na kwa wakati gani na mgeni yoyote anayefuata maelekezo hayo anakuwa amejiweka katika mazingira mazuri ya kufikia malengo yake aliyojiwekea kabla ya safari.
Wapo baadhi ya wageni wachache ambao hupuuza maelekezo ya waongozaji wageni na hawa hujikuta wakiishia njiani ama kupatwa na matatizo ya kiafya ikiwamo kupungukiwa na hewa ya oksijeni .
Alfred Kibiriti ni mmoja wa waongozaji wageni nguli anayehudumu katika nafasi hiyo kwa muda mrefu kutoka kampuni ya uwakala wa utalii ya African Scenic ,anasema mgeni yoyote anayeshindwa kufuata maelekezo ya waongozaji wageni anajiweka katika hatari ya kushindwa kufanya vizuri.
Anasema waongozaji wageni ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wamepewa mafunzo maalumu na maofisa wa hifadhi hiyo ya jinsi ya kuongoza wageni hivyo wanao utaalamu wa kutosha katika masuala ya kuongozaji wageni.
"Guide amefundishwa taratibu zote za uongozaji,wanaokuja kupanda mlima na kujiona wana nguvu na kukiuka kanuni,taratibu na sheria zilizowekwa na ambazo guide anazitoa kwa wageni,ndiyo hao wanashindwa kufanya vizuri,ni mhimu wakafuata maelekezo ya guide",anasema
mchango wa wapishi kwa wageni mlima
kilimanjaro.
Hili ni kundi jingine mhimu sana katika kufanikisha safari ya wageni kupanda mlima kilimanjaro kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho kwani suala la lishe ni moja ya nguzo mhimu kwa mgeni katika kumjenga kiafya .
Kwa wageni wanaotumia lango kuu la marangu katika kupanda mlima huo,kazi ya mpishi huanzia kituo cha kwanza cha Mandara kilichopo umbali wa mita 2,720 kutoka usawa wa bahari kabla ya kuelekea kituo cha pili cha Horombo ambacho kipo umbali wa mita 3,720 kutoka usawa wa bahari.
Kwenye kituo hicho cha Horombo mgeni hukaa hapo kwa siku mbili na kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa kilometa 3.4 kuelekea kwenye mwamba wa jiwe mfano wa mnyama aina ya pundamilia maarufu kwa jina la Zebra Rocks.
Hapo wageni mbali mbali hujumuika na kupiga picha za kumbu kumbu na lengo la mazoezi hayo ni kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa na kujiweka fiti kabla ya kuanza safari kuelekea kilele cha Volkano tuli cha Kibo kilichopo umbali wa mita 4,720 kutoka usawa wa bahari.
Ukiwa hapo Kibo mpishi ana makujumu mawili la kwanza ni kuandaa chai ya jioni kwa ajili ya wageni ambao hufika muda wa jioni na mara baada ya zoezi hilo kukamilika anawajibika kuingia jikoni tena kwa ajili ya kuandaa chakula cha usiku kabla ya wageni kuanza safari ya kwenda kilele cha uhuru.
Mgeni anaporejea kutoka kilele cha uhuru
hadi kituo cha Kibo,sharti apate chai na chakula cha mchana kabla ya kuendelea
na safari hadi kituo cha Horombo ambako anapata mapumziko kabla ya siku
inayofuata kurejea hadi lango kuu la marangu.
Wapagazi,a.k.a wagumu
Wanaitwa wagumu kutokana na ugumu wa kazi wanayoifanya katika kuwahudumia wageni kuanzia siku ya kwanza ya kupanda mlima Kilimanjaro hadi wanaporejea safari yao ya siku sita ama zaidi kulingana na ratiba ya mgeni.
Kazi yao kubwa ni kubeba mabegi makubwa yaliyosheheni nguo maalum za kuvaa wageni wakati wa kupanda mlima huo,chakula kwa ajili ya wageni na mabegi ya nguo zao za kujisitili wawapo ndani ya hifadhi hiyo.
Kabla ya kuanza safari,mizigo yao hupimwa
kwa ajili ya kuhakiki uzito unatostahili kwa mujibu wa kanuni na taratibu
zilizowekwa na shirika la hifadhi za taifa tanzania(Tanapa) ambazo zinaelekeza
uzito unaostahili kwa kila mpagazi kuwa ni kilo 20 na si zaidi ya hapo.
Mbali na mabegi ya nguo za wageni,vyakula na nguo zao,wagumu hawa hubeba majiko kwa ajili ya kupikia chakula cha wageni na majiko yanayokubalika kwa mujibu wa taratibu za hifadhi ni majiko ya gesi pamoja na maji ya kupigia.
Hawa ndiyo wagumu,mizigo wanayobeba na mishahara wanayolipwa ni mbingu na dunia
Hawa si watu wa mchezo mchezo,ukikutana
nao njiani na aina ya mwendo wanaotembea huwezi ukaamini kuwa mzigo aliobeba
una kilo 20,milima na mabonde kwao ni sawa na kifungua kinywa,wanakimbia ajabu
na huwezi ukashindanana nao,hao ndiyo wagumu wa ukweli.
Pamoja na majukumu hayo mazito,makundi
haya ambayo ni mhimili mkubwa katika kufanikisha safari za wageni ndani ya hifadhi
hiyo,malipo wanayolipwa na mawakala wa utalii hayaendani na ugumu wa kazi
wanayoifanya.
Ni malipo ambayo yanadhalilisha utu
wao,lakini wanalazimika kuyakubali kutokana na umaskini wao wa kipato kwani upo
usemi usemao 'ukisusa wenzako twala',maana yake ni kwamba ukisusia malipo hayo
wapo wenzako wenye shida zaidi watayapokea.
Licha ya malipo hayo kuwa kiduchu,bado wapagazi wanateswa na baridi kali ndani ya mlima kilimanjaro kutokana na kutokuwa na mavazi maalumu ya kujikinga na baridi na hulazimika kunywa pombe inayofungashwa kwenye viroba kama moja ya njia ya kujikinga na baridi.
Kwa mujibu wa tangazo la serikali(GN)
namba 228 la mwaka 2008,bunge liliidhinisha malipo ya dola 20 kwa siku kwa
mwongozaji watalii,dola 15 kwa siku kwa mpishi na dola 10 kwa siku kwa mpagazi.
Hata hivyo chama cha wapagazi,kimelalamika
kuwa tangu tangazo hilo la serikali kutolewa,makampuni ya uwakala wa utalii yamekuwa hayalipi viwango
hivyo na huwalipa wapagazi,waongazaji watalii na wapishi malipo duni ambayo
hayaendani na ugumu wa kazi yao. 
Je vyama vya wapagazi vinamchango gani
katika kupigania maslahi ya wapagazi mlima Kilimanjaro?
Fuatilia Makala ijayo ambayo itakuja kujibu
hoja hizi kutoka kwa viongozi wa vyama vya wapagazi KPA na TPO






0 Comments