MOSHI-KILIMANJARO
SERIKALI imetoa wito kwa mafundi ujenzi kuwa waaminifu na kuacha tabia ya udokozi pale wanapotekeleza majukumu yao ya ujenzi ili kuendelea kuaminiwa na kupata kazi Zaidi.
Wito huo umetolewa mjini moshi na Afisa tawala wilaya ya Moshi,Theresia Mmbaga kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Moshi,Godfrey Mnzava katika hafla fupi iliyoandaliwa na kampuni ya FAJU45 ya mkoani Arusha hafla iliyokuwa mahususi kwa ajili ya kutambulisha bidhaa zake kwa mafundi ujenzi na mafundi rangi .
Alisema
kumekuwepo na kesi nyingi za mafundi kuiba material ya wateja wao wanapokuwa
kwenye majukumu yao ya ujenzi na kukitaka Chama cha mafundi rangi na
ujenzi(CHAMARUKI)kuangalia mienendo ya wanachama wao.
Aliwataka mafundi hao kujisajili kwenye mfumo wa NEST ambao ni mfumo unaowawezesha mafundi wengi kuomba kazi za serikali huku pia akiwataka kupeleka taarifa zao kwenye halmashauri za wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa kazi.
Alisema ni wajibu wa mafundi kutafuta watalamu wa kuwaandikia michanganuo ya kuomba kazi serikali ili nao waweze kunufaika na kandarasi zinazotolewa serikalini.
Mwenyekiti wa CHAMARUKI wilaya ya Hai,Yohana Severini alisema mapatano ya mafundi na wateja wao yasiyozingatia taratibu sahihi yanachangia mafundi wengi kujihusisha na wizi huku pia akidai mafundi wengi hawana uelewa wa namna ya kuomba kazi za serikali.
Katika hatua nyingine CHAMARUKI kimeitikia ombi la kamanda wa polisi wilaya ya moshi(OCD) na sasa kinakamilisha mchakato wa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la polisi wilaya.
Katibu mtendaji wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro, Casmiry John Toto, alisema ukarabati huo unatokana na ombi la kamanda wa polisi wilaya ya Moshi (OCD), ambaye aliomba msaada wa mafundi kutoka chama hicho kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na kampuni ya FAJU 45 CO. LTD, kazi hiyo ya ukarabati itatekelezwa kwa pamoja ambapo CHAMARUKI watatoa nguvu kazi, huku kampuni hiyo ikiahidi kuchangia fedha na vifaa vitakavyohitajika.
Mtendaji Mkuu wa FAJU 45 CO. LTD, Omari Mohamed Ndwatta, alitoa rai kwa mafundi ujenzi na mafundi rangi kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika shughuli zao kama mkakati mojawapo ya kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa na watanzania wenzao.Kabla ya hafla hiyo,kampuni hiyo na wadau wengine walitembelea kituo cha kulelea watoto wanaoishi mazingira magumu cha Faraja kilichopo Rau mjini moshi na kutoa misaada ya kibinadamu ikiwamo sabuni,mchele,mikate na mafuta.





0 Comments