ADAM BEST SIMBA ANENA:CCM HANA HOFU NA USHINDI OKTOBA 29,ATAKA WANANCHI WAJITOKEZE KWA WINGI KUPIGA KURA

  




Mjumbe wa kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Kilimanjaro,Adam Best Simba(kushoto)akinadi mgombea wa kiti cha Udiwani kata ya Bondeni Mnaispaa ya moshi,Haji Fundi Haji wakti wa mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Bondeni.

 

              MOSHI-KILIMANJARO.

MJUMBE wa kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Kilimanjaro na mratibu wa kampeni wa CCM mkoa ,Adam Best Simba amewataka wananchi wa jimbo la Moshi mjini na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu oktoba 29 mwaka huu ili kukipa ushindi chama hicho.

Best Simba alitoa wito huo kwenye mkutano wa kampeni za chama hicho Jimbo la Moshi mjini zilizofanyika kwenye kata ya Bondeni Manispaa ya Moshi ambako alitumia mkutano huo kumnadi mgombea wa kiti cha ubunge Ibrahim Shayo na mgombea udiwani Kata ya Bondeni,Haji Fundi Haji.

Akizungumza katika mkutano huo kada huyo wa CCM na mfanyabiashara maarufu nchini,alisema hana shaka na ushindi wa Chama Cha Mapinduzi hapo oktoba 29 mwaka huu kuanzia nafasi ya Rais,Ubunge hadi kwa madiwani na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

“Naomba niwahakikishie wananchi kwamba sina shaka na ushindi wa Chama cha Mapinduzi jambo la muhimu ni nyie mjitokeze kwa wingi kupiga kura oktoba 29,nimekuja hapa kumwombea kura za kishindo mgombea wetu wa urais na pia nimekuja kuwanadi mgombea wetu wa kiti cha ubunge pamoja na mgombea wa nafasi ya udiwani”,alisema.

'Mwamba' Haji Fundi Haji(kulia)akiomba kura za udiwani kwa wananchi wa kata ya Bondeni Manispaa ya moshi  kwenye mkutano wa Kampeni uliofanyika kwenye kata hiyo

Akizungumza katika mkutano huo mgobmea wa kiti cha udiwani,Haji Fundi Haji alisema kata ya Bondeni ambayo ni eneo la kibiashara kutokana na kuwa na masoko mawili makubwa,Mbuyuni na manyema inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo suala la miundombinu ya maji taka pamoja na ukosefu wa    taa za barabarani hali inayochangia uwepo wa matukio ya kiharifu.

Aliahidi kujenga ofisi za serikali za mitaa kwa ajili ya kuwarahisisha huduma wananchi wa kata hiyo endapo atachaguliwa kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi katika Baraza la madiwani pamoja na kujenga ofisi itakayoshughulikia masuala ya migogoro ya Ardhi kwa wananchi hao badala ya kutumia muda mwingi kufuata huduma hiyo baraza la ardhi la wilaya.

Alipongeza mfanikio ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais,Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake katika karibu zote kuanzia suala la Afya,Elimu na miundombinu ya barabara ikiwamo mradi wa Treni ya mwendo kasi (SGR)kutoka Dar es salaam hadi Dodoma mradi aliodai Rais aliukuta ukiwa aslimia 30 ya ujenzi.

Akimwombea kura mgombea wa kiti cha Ubunge Jimbo la Moshi Mjini,Ibrahim Shayo maarufu kwa jina la ‘Ibra Line’,Haji Fundi Haji alisema mgombea huyo amefanya mambo mengi  mazuri kwa wananchi wa Moshi mjini kabla hajawaza kuwa mbunge na kuwaomba wampe kura nyingi katika uchanguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani hapo Oktoba 29 mwaka huu.

“Ndugu zangu wananchi wa kata ya Bondeni,siku zote wema hulipwa kwa wema,Ibra Line amefanya mengi kwa wananchi wa moshi mjini na nyie ni mashahidi,naombeni sana oktoba 29 twende tukalipe wema kwa ndugu yetu Ibra Line kwa kumpa kura nyingi za kishindo”,alisema.


Kwa upande wake ,Irahim Shayo ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini katika sekta ya usafrishaji na sekta ya mafuta alisema anajua changamoto za wananchi wa kata ya Bondeni ambao wengi wao ni wafanyabiashara kama alivyo yeye.

“Ninajua changamoto zenu kama wafanyabiashara wenzangu maana huko ndiko nimetoka,naomba niwahakikishiek uwa kama mtanichagua kuwa mbunge wenu,hakuna mfanyabiashara yoyote atakayeondolewa kwenye maeneo yenu”,alisema.

Alionyesha pia kukerwa na mfumo wa majitaka kwa wananchi wa kata ya Bondeni na maeneo mengine ya mji wa Moshi na kuahidi kushughulikia kero hiyo atakapochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Moshi mjini kwenye uchanguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema changamoto hiyo ya mfumo wa majitaka moshi mjini ni mfumo wa zamani ambao kwa sasa haufai kutokana na ongezeko la watu na kuahidi kushirikiana na mamlaka ya Majisafi  na Uondoshaji majitaka moshi mjini(MUWSA)kushughulikia changamoto hiyo.



Post a Comment

0 Comments