Makala hii imeandaliwa na Bahati Nyakiraria na Charles Ndagulla
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania(Tanapa)limezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Uendeshaji wa Kampuni
Tanzu ya Uwekezaji ya Tanapa Investment
Limited – TIL) na kufungua ukurasa mpya katika historia ya usimamizi wa
rasilimali, uwekezaji na uendelevu ndani ya TANAPA.
Tukio hilo lililoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
wa TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Marwa Waitara hivi karibuni,
limeonesha dhamira ya dhati ya shirika hilo kuhakikisha usimamizi makini wa
miradi yake ya kibiashara sambamba na kuongeza mchango wa uhifadhi katika
uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Jenerali Waitara aliipongeza Bodi hiyo kwa kuaminiwa na kukabidhiwa jukumu muhimu la kusimamia TIL, kampuni iliyoanzishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi, ubunifu, na tija katika uwekezaji wa TANAPA.
Waitara alisisitiza
kuwa uteuzi wa wajumbe hao ni matokeo ya kuamini uwezo wao wa kitaaluma na
uzoefu wao katika masuala ya uongozi, uchumi, uwekezaji, na uhifadhi.
Jenerali Waitara alitoa wito kwa bodi hiyo kuimarisha
misingi ya uwajibikaji, weledi na uwazi katika kutekeleza majukumu yake na
kwamba TIL inahitaji kuongozwa kwa
mtazamo mpana utakaowezesha kampuni kujiimarisha katika ushindani wa
kibiashara, hususan katika mazingira ya sasa ambapo miradi mingi ya sekta ya
umma inasisitiza kutumia utaalamu wa ndani ili kupunguza gharama na kuongeza
ufanisi.
Katika hotuba yake, alieleza kuwa bodi inatarajiwa
kuanzisha na kusimamia miradi ya kimkakati itakayochochea ukuaji wa mapato ya
TANAPA bila kutegemea vyanzo vya jadi pekee.
Hii inajumuisha miradi ya miundombinu ya utalii, majengo,
uwekezaji wa kiteknolojia, na huduma shirikishi zinazolenga kuboresha uzoefu wa
watalii katika hifadhi za taifa.
Serikali, kupitia Bodi ya Wadhamini na menejimenti ya TANAPA, imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha uhifadhi na kutunza maliasili za taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(Tanapa),Mkuu wa Majeshi Mstaafu ,Jenerali George Mwita Waitara
Jenerali Waitara amesema
wajumbe wa bodi wanategemewa kuwa chachu ya kuleta ubunifu na mtazamo wa
kimkakati katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dira hiyo
inasisitiza uhifadhi endelevu, matumizi ya teknolojia, na uwekezaji katika
miradi yenye manufaa kwa jamii.kwa mantiki hiyo, TIL inapaswa kuwa mfano wa
taasisi za serikali zinazochanganya biashara na uhifadhi kwa ufanisi unaoleta
matokeo halisi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, CPA Mussa
Nasoro Kuji, alisisitiza kuwa uzinduzi wa bodi hiyo unaendana moja kwa moja na
juhudi za serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alibainisha kuwa serikali imeweka mazingira bora ya
uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi, hasa katika sekta ya utalii na uhifadhi
ambazo zinazidi kuwa nguzo muhimu za mapato ya taifa.
Aidha, alieleza kuwa TANAPA imejipanga kikamilifu
kuhakikisha kuwa mageuzi yanayotekelezwa na serikali yanaenda sambamba na
ukuaji wa sekta ya uhifadhi kwa kuanzisha miradi inayochochea maendeleo ya
kijamii na kiuchumi.
CPA Kuji aliongeza kuwa TIL inayo nafasi muhimu katika
kuhakikisha kwamba miradi ya TANAPA inatekelezwa kwa ufanisi unaotakiwa, ikiwa
ni pamoja na kuongeza thamani ya maeneo ya hifadhi, kuboresha miundombinu na
huduma zinazowavutia watalii wa ndani na nje.
Aidha, alisisitiza kuwa uwekezaji utakaofanywa kupitia TIL
utapaswa kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya uhifadhi na maendeleo
ya jamii zinazozunguka hifadhi.
Naye Mtendaji Mkuu wa TIL, Mhandisi Dkt. Richard Matolo,
aliweka wazi dira ya kampuni hiyo huku akitoa msisitizo juu ya matumizi ya
utaalamu wa hali ya juu na teknolojia katika kuendesha miradi ya ukandarasi.
Dkt. Matolo alieleza kuwa TIL imejiandaa kikamilifu kuleta
mapinduzi katika sekta ya ukandarasi kwa kuhakikisha miradi yote inakamilika
kwa wakati, kwa ubora wa juu, na kwa gharama zinazowiana na thamani ya kazi.
Kwa mtazamo wake, matumizi ya teknolojia za kisasa sio tu
yataboresha ufanisi wa kazi, bali pia yatapunguza utegemezi wa wakandarasi
kutoka nje ya taasisi.
Hii itasaidia TANAPA
kuwa na udhibiti mkubwa wa miradi, kupunguza gharama za uendeshaji, na
kuimarisha uwezo wa ndani wa kitaalamu.
Mbali na hilo, Dkt. Matolo alisisitiza kuwa TIL itakuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa miradi inaendana na viwango vya
kimataifa vya ukandarasi na ujenzi, hatua itakayoongeza hadhi ya kampuni katika
soko la ndani na nje.
Kwa ujumla, uzinduzi huu umeleta matumaini makubwa kwa
wadau wa uhifadhi, utalii na uwekezaji nchini.ni hatua muhimu katika kuelekea
kujenga taasisi imara ya kibiashara ndani ya TANAPA ambayo si tu itahakikisha
mapato endelevu, bali pia itachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uhifadhi wa
rasilimali za taifa na kuboresha ustawi wa jamii.
TIL, ikiwa na bodi mpya yenye uzoefu na maono mapana,
inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuleta mageuzi chanya katika uwekezaji
na utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Huu ni mwanzo mzuri unaoashiria
mustakabali wenye matumaini makubwa kwa sekta ya uhifadhi na tasnia ya utalii
kwa ujumla.



0 Comments