MRAJIS USIKUBALI MALI ZA USHIRIKA KIRIMA BORO AMCOS ZIGEUZWE VIHAMBA

 JENGO LA MAKAO MAKUU YA KNCU KAMA LINAVYOONEKANA KWA MBALI 

 

                                          KILIMANJARO

WANACHAMA wa Chama cha msingi cha ushirika wa mazao(AMCOS)cha Kirima Boro kilichopo wilaya moshi mkoani Kilimanjaro wamepaza sauti kuhusiana na mwenendo usioridhisha wa viongozi wa Bodi ya uangalizi ya chama hicho kudaiwa kuuza mashamba yanayomilikiwa na chama hicho kwa watu binafsi,wakiwamo wanasiasa,wafanyabiashara na watu wengine.

Kwamba Bodi hiyo ambayo imekuwa madarakani kwa miaka mine kinyume na ilivyokuwa ya kuwa madarakani kwa siku 90 ,imekuwa ikifanya yale ambayo hayakuwa makusudio ya uwepo wake.

Mheshimiwa mwenyekiti Bodi ya caretaker ya  KIRIMA BORO AMCOS imefanya ufisadi mkubwa kuuza mali za Ushirika likiwemo ekari 7 za shamba la Sangiti. Nilishirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Boro Laurent Meja kwenda hadi TAKUKURU kutoa taarifa za Caretaker kukaa madarakani zaidi ya miaka 4 badala ya siku 90” 

“Mwenyekiti, mali nyingine zilizouzwa bila ridhaa ya Mkutano Mkuu ni jembe la trekta na trailer,hakuna ukaguzi wa Mahesabu ya Ushirika ” 

“ Ninayo taarifa kuwa Ukaguzi wa mwisho ni Mwaka 2021/2022 ambao umefichwa na Afisa Ushirika kwa sababu kuna taarifa ya ufisadi wa fedha nyingi zimeliwa na Wajumbe wa Bodi iliyokuwa chini ya .......(anataja jina)” 

Huu ni ujumbe uliotumwa kwa kiongozi mmoja wa chama cha mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro  kutoka kwa mmoja wa wanachama wa chama hicho akimuomba aingilie kati kuunusuru ushirika huo ili viongozi hao wasiendelee kuuza mali za ushirika.

 Kwa faida ya wasomaji wetu,mwaka 2019 serikali ya awamu ya tano ilianzisha oparesheni ya kurejesha mali za ushirika zilizokuwa zimeuzwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo kwa watu binafsi na wafanyabiashara wakubwa .

Oparesheni hiyo ilivikumba vyama vikuu vya KNCU(Kilimanjaro),SHIRECU(Shinyanga),NYANZA(Mwanza) na maeneo mengine ambako tume ya uchunguzi iliyoundwa na ofisi ya waziri mkuu wakati huo ilifichua ufisadi mkubwa wa mali za wanaushirka.

Mkoani Kilimajaro ripoti ya ukaguzi  ikafichua mauzo tata ya shamba kubwa la kahawa la Gararagua   lililopo Wilaya ya Siha mali ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) ambako tume ilibaini liliuzwa  chini ya thamani halisi ya bei ya soko, pamoja na kutokujulikana zilipo ekari 2,000.

Shamba hilo liliuzwa mwaka 2017 na KNCU kwa dola za Marekanai milioni 4.2 sawa na Sh bilioni 9.24,(kwa wakti huo) ikiwa ni mkakati wa chama hicho kujinasua na madeni makubwa likiwamo deni la Sh bilioni 5.2 ambalo chama hicho kilikuwa kinadaiwa na Benki ya CRDB.

Liliuzwa kwa Kampuni ya Tanbreed/Africado baada ya chama hicho kuvunja mkataba na mwekezaji aliyekuwa akiendesha shamba hilo Kampuni ya Ocean Link Shipping Services Limited na kukubali kumlipa fidia ya Sh bilioni 2.9 malipo ambayo yanadaiwa kugubikwa na utata pia.

KNCU ilivunja mkataba na mwekezaji huyo uliokuwa wa miaka 30 na ambao ungefikia ukomo mwaka 2030, hivyo mwekezaji huyo alilipwa fidia hiyo ya miaka 16 iliyobaki kulingana na mkataba wake kama angeendelea na uwekezaji.

Hata hivyo ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro ilibaini madudu mengi kwenye mchakato mzima wa kuuzwa kwa shamba hilo ambalo kwa mujibu wa ripoti hiyo lilikuwa na ukubwa wa ekari 5,414 mwaka 1980.

Madudu hayo ndiyo yakaisukuma serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa(wakati huo) kuunda timu ya kuchunguza uuzwaji wa shamba hilo na matokeo ya uchunguzi huo ‘yakawasukuma’ ndani waliokuwa viongozi wa Bodi ya KNCU.

Mwenyekiti wa bodi hiyo na makamu wake pamoja na aliyekuwa Meneja wa KNCU, Honest Temba wakafunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia KNCU hasara ya Sh bilioni 2.9.     

Mbali na hao, walikuwemo pia  viongozi wa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing (TCCCo), Maynard Swai, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi na Andrew Kleruu aliyekuwa meneja wa kiwanda hicho nao walifikishwa mahakamani wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya.kwa  kununua mtambo  wa kukoboa kahawa kutoka Kampuni ya Brazafric ya Brazil bila kufuata taratibu na kuisababishia TCCCo hasara ya Sh bilioni 1.67.

  Nimerejea ripoti hii ili jamii ijue kuwa mali hizi za ushirika si vihamba kwamba walioko madarakani wanagawa kama wanagawia familia zao(vihamba)na nimuombe mrajis wetu Dkt.Benson Ndiege asikubali mali za ushirika kuuzwa kama mali za ukoo.

Kwa wanaomfahamu Dkt.Ndiege ni mtu wa msimamo,ni kiongozi asiyeweza kufumbia macho ufisadi wa mali za ushirika,ni mtu ukimwamsha usiku anawaza ushirika,ukisema nae anawaza ushirika ni jukumu letu kumuunga mkono ili kukomesha ufisafi wa aina hii

HAWA NI WANANCHI WA KIRIMA BORO MOSHI VIJIJINI WALIPOFIKA MJINI MOSHI KUPAZA SAUTI KUTAKA UUZWAJI WA SHAMBA LA USHIRIKA KIRIMA BORO AMCOS UKOMESHWE

Post a Comment

0 Comments